Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahofia ujenzi zaidi wa makazi ya Walowezi Israel

Ban ahofia ujenzi zaidi wa makazi ya Walowezi Israel

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu wamejadili juhudi zinazoendelea za kusukuma mbele mchakato wa amani ,huku Ban akielezea hofu yake juu ya mipango ya ujenzi wa makazi zaidi ya walowezi Mashariki mwa Jerusalem.

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba ni muhimu kumaliza mtafaruku wa sasa wa kidiplomasia, kuanza majadiliano na kuleta matokeo mazuri ya amani. Ban na Netanyahu pia wamejadili ripoti ya karibuni ya azimio namba 1701 la baraza la usalama yenye lengo la kumaliza mgogoro baina ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon.

Mengineyo yaliyojitokeza kwenye mjadala wao ni pendekezo la karibuni kuhusu suala la kijiji cha Ghajar kwenye eneo la Kaskazini linalokaliwa na Israel. Katibu Mkuu ameelezea matumaini kwamba Israel itachukua hatua zaidi kurahisisha hali ya watu na mizigo kuingia na kutoka Gaza. Kwa pamoja wamethamini hali ya ukanda mzima ikiwemo Iran.