Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya kupungua utapia mlo, njaa bado ni tatizo:FAO

Licha ya kupungua utapia mlo, njaa bado ni tatizo:FAO

Umoja wa Mataifa leo unasherehekea siku ya kimataifa ya chakula ambayo kwa kawaida huadhimishwa tarehe 16 Oktoba duniani kote.

Wakati shirika la chakula na kilimo FAO linakadiria kuwa idadi ya watu wenye utapia mlo imepungua kwa kiasi duniani kote kutoka watu bilioni moj mwaka jana, lakini bado watu milioni 925 inakadiriwa wanaendelea kukabiliwa na njaa na utapia mlo.

Siku hii ya chakula duniani kila mwaka huadhimishwa na FAO na nchi 150 duniani kote na inatoa fursa kutanabaisha hali isiyokubalika kwa mamilioni ya watu kukabiliwa na baa la njaa na utapia mlo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni tuungane dhidi ya njaa, ikionyesha umuhimu wa nchi, mashirika ya jumuiya za kijamii, sekta binafsi na watu binafsi katika ngazi zote kuendelea kuchukua hatua kukomesha njaa, umasikini uliokithiri na utapia mlo.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York kunafanyika hafla maalumu kuadhimisha siku hii ikiongozwa na mkurugenzi mkuu wa FAO, na ujumbe maalumu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa baraza kuu la Umoja wa mataifa.