Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID inahofia kukamatwa kwa waandishi Khartoum

UNAMID inahofia kukamatwa kwa waandishi Khartoum

Mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwenye jimbo la Darfur Sudan UNAMID umesema unatiwa hofu na taarifa za kufungwa ofisi za radio mjini Khartoum na kukamatwa kwa waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu.

UNAMID imetoa wito wa kuwaheshimu waliowekwa mahabusu na kukamatwa na pia imeelezea matumaini ya kupata suluhisho la suala hilo kwa njia ya amani. Kwa mujibu wa duru za habari wanaharakati 10 kutoka Darfur akiwemo mwanasheria Abderahmane Gassim na wajumbe tisa wa shirika la kupigania haki za binadamu la eneo hilo walikamatwa tangu Jumamosi iliyopita mjini Khartoum.

UNAMID ilianzishwa na baraza la usalama mwaka 2007 ili kuwalinda raia kwenye jimbo la Darfur ambako inakadiriwa watu 300,000 wameuawa na wengine milioni 2.7 wamelazimika kuzikimbia nyumba zao kutokana na machafuko yaliyozuka 2003 kati ya makundi ya waasi na majeshi ya serikali yanayosaidiwa na wanamgambo wa Janjaweed.