Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri mkuu wa Somalia aahidi kukomesha matumizi ya watoto jeshini

Waziri mkuu wa Somalia aahidi kukomesha matumizi ya watoto jeshini

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa masuala ya watoto kwenye migogoro ya kutumia silaha Radhika Coomaraswamy amekutana jana na waziri mkuu mpya wa Somalia Mohammed Abdullahi Mohammed mjini Moghadishu.

Katika majadiliano yako waziri mkuu ameahidi kwamba serikali yake itatokomeza kitendo cha kuwatumia watoto katika vita nchini Somalia, akitambua kwamba matumizi ya watoto jeshini ni hayapasi na amekubali kuanzisha kitengo kitakachokuwa kikiwasilisha taarifa moja kwa moja kwake ambacho kitafanya kazi na Umoja wa Mataifa kuhakikisha mipango inaidhinishwa na kutia saini makubaliano rasmi ambayo yatasaidia kuwapata na kuwaachilia askari watoto.

Kuahidi kumaliza kitendo cha kuwaingiza jeshini watoto nchini Somalia ni hatua ya kwanza inayokaribishwa kama kukubali kwake kuweka saini mipango ambayo itazuia watoto kuchukuliwa na kutumika kama wanajeshi na serikali ya mpito ya nchi hiyo TFG, amesema bi Coomaraswamy.

Ameongeza TFG na wanamgambo ambao ni washirika wao wamekuwa kwenye orodha ya kutajwa na kuaibishwa ya Katibu Mkuu kwa kuwafunza na kuwatumia watoto jeshi katika miaka mitano mfululizo na imekuwa ikichukuliwa kama mkiukaji mkubwa wa mkataba wa kutotumia watoto vitani.

Amesema ni matumaini yake kwamba niya na waziri mkuu na utekelezaji wa vitendo utasaidia hatimaye kuiondoa Somalia katika orodha hiyo. Na katika mkutano wake na mkuu wa vikosi vya kulinda amani vya Muungano wa Afrika AMISOM kamnda Nathan Mugisha, Bi Coomaraswamy ameelezea hofu yake juu ya mauji yanayoendelea ya raia na hasa watoto, kwa magruneti yanayovurumishwa bila mpango.

Lakini amehakikishiwa na kamanda Mugisha kwamba sheria na hatua zitachukuliwa kuzuia vifo zaidi vya raia wakiwemo watoto. Bi Coomaraswamy jana pia alikutana na Rais wa Somaliland na kumpongeza kwa ushindi wa uchaguzi wa hivi karibuni, na leo ametembelea kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bossaso na kuzungumza na baadhi ya wanawake na watoto.