Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfanyabiashara wa Rwanda afungwa miaka 30 kwa mauaji ya kimbari

Mfanyabiashara wa Rwanda afungwa miaka 30 kwa mauaji ya kimbari

Mfanyabiashara wa zamani wa Rwanda amehukumiwa kwenda jela miaka 30 kutokana na makosa ya ukatili dhidi ya ubinadamu yaliyotendeka Rwanda mwaka 1994 wakati wa mauaji ya Kimbari.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa mauaji ya Rwanda ICTR iliyoko Arusha Tanzania imemkuta na hatia Gaspard Kanyarukiga ya kupanga mauaji ya Watutsi kanisani Nyange wakati wa siku 100 za mauaji ya kimbari. ICTR imesema kusambaratishwa kwa kanisa la Nyange kulifanyika kama sehemu ya mashambulizi yaliyopangwa dhidi ya Watutsi.

Pia mahakama hiyo imemkuta na hatia ya kushiriki mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa Kitutsi kwa lengo la kuwamaliza kabisa jambo ambalo ni kola uhalifu dhidi ya ubinadamu. Bwana Kanyarukiga alikamatwa nchini Afrika ya Kusini July 2004, na alikana mashitaka yote dhidi yake.