Skip to main content

Rais na spika wa bunge Somalia malizeni tofauti zenu:Mahiga

Rais na spika wa bunge Somalia malizeni tofauti zenu:Mahiga

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Augustine Mahiga leo amefanya mkutano na Rais wa serikali ya mpito ya Somalia Sheikh Sharif Ahmed na spika wa bunge la nchi hiyo Sharif Hassan Sheikh Aden kwenye uwanja wa ndege wa Moghadishu.

Mazungumzo yao ni kuhusu mvutano baina ya viongozi hao wawili uliosababisha kuchelewa kuidhinishwa na bunge waziri mkuu mpya aliyeteuliwa hivi karibuni. Mahiga amekutana na Rais na spika wa bunge ili kutatua mvutano huo amesema Yasin Mohamed mmoja wa wabunge wa Somalia.

Baada ya mkutano na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Rais Sharif na spika wameketi na kujadili njia za kutatua mtafaruku wao. Mahiga amewaomba viongozi hao kuunda serikali mpya kwa amani na utulivu na kuainisha ajenda za nini cha kufanya katika miezi michache iliyosalia ya kipindi cha mpito kabla hakijaisha hapo Agosti mwakani.