Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Drogba aanza kampeni ya uchaguzi huru na wa haki duniani

Drogba aanza kampeni ya uchaguzi huru na wa haki duniani

Mwanasoka mashuhuri duniani Didier Drogba leo ameanza kampeni ya kimataifa ya kutanabaisha jinsi uchaguzi huru na wa haki unavyoweza kuwa nyenzo muhimu ya kuzitoa nchi masikini kabisa duniani kutoka kwenye ufukara huo.

Drogba ambaye aliongoza timu ya nchi yake ya Ivory Coast kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya kombe la dunia 2006 amezindua bango lenye ujumbe muhimu kwa wapiga kura usemao ‘jitupe uwanjani na kuwa mchezaji, jiandikishe, piga kura, usikike" Drogba amesema ili maendeleo yaweze kupatikana lazima tuhakikishe kunakuwa na uchaguzi huru wa wazi na wa haki, ameongeza kuwa anaamini utawala bora unaweza kuziondoa nchi katika mzunguko wa umasikini hasa wapiga kura, na wanasiasa watakapotimiza wajibu wao.

Amesema lengo la kampeni yake ni kuchangia kuwepo kwa demokrasia barani Afrika hasa ukizingatia nchi nyingi zinaelekea uchaguzi hivi karibuni. Bango la kampeni hiyo linazindiliwa mjini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako chaguzi tisa zimepangwa kufanyika katika miaka mitatu ijayo ukiwepo wa Rais, wabunge na madiwani.

Drogba ni mmoja kati ya mablozi mashuhuri wema wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo UNDP, wakiwemo wanamichezo Ronaldo, Zinedine Zidane, Maria Sharapova na mcheza filamu Antonio Banderas.