Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urithi wa sauti na picha ni muhimu:UNESCO

Urithi wa sauti na picha ni muhimu:UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO leo katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya urithi wa sauri na picha limetoa wito wa kuongeza juhudi za kuhifadhi kumbukumbu muhimu zilizoko katika njia ya sauti na picha.

Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Irina Bokova ameonya kwamba urithi wa dunia wa sauti na picha uko hatarini. Ameongeza kuwa kumbukumbu za vitu kama filamu, video, redio na sauti nyingine zilizorekodiwa zinatoa hisia na ubunifu na ni ushahidi wa historia ya binadamu.

Amesema hatari ya kumbukumbu hiyo ni kubwa kwani hadi sasa nyingi zimepotea kutokana na kupuuzwa, kuharibika na tekinolojia duni ya kuhifadhi jambo ambalo litatia dosari katika kumbukumbu ya historia ya mwanadamu na dunia kwa ujumla.

Bi Bokova ameonya kwamba vizazi vijavyo huenda visipate fursa ya kushuhudia nyakati muhimu za kihistoria kama binadamu wa kwanza kutua mwezini mwaka 1969 au Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Nelson Mandelea akifunguliwa kutoka gerezani mwaka 1990. Amesema kwa kulitambua hilo UNESCO na mashirika mengine wamechukua hatua za kuwa msitari wa mbele kuhifadhi kumbukumbu hizo.