Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yasitisha tuzo kwa Rais wa Equatorial Guinea

UNESCO yasitisha tuzo kwa Rais wa Equatorial Guinea

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Irina Bokova leo amesitisha tuzo aliyokuwa apewe Rais wa equatorial Guinea kusubiri majadiliano yanayoendelea kutokana na pande zote husika na tuzo hiyo.

Wajumbe 58 wa bodi ya tuzo hiyo wamesema majadiliano kuhusu tuzo kwa bwana Obiang Nguema Mbasogo ambayo ni ya utafiti wa kimataifa wa kisayansi yataendelea kwa heshma hadi muafaka utakapopatikana.

Bi Bokova amesema uamuzi wa kusitisha tuzo hiyo ni wa wajumbe na anauheshimu. Tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 2008 kwa lengo la kutunukia miradi na shughuli za watu binafsi, taasisi au mashirika mengine kwa utafiti ambao utaimarisha hali ya maisha ya binadamu.

Mwezi uliopita Equatorial Guinea ilitaka tuzo hiyo iendelee mara moja ikidai kwamba imesitishwa tu kwa sababu aliyetunukiwa ni kiongozi wa Afrika. Wawakilishi wa baadhi ya nchi hata hivyo wameishutumu serikali ya bwana Obiang Nguema ambaye amekuwa madarakani tangu 1979 kwa ukiukaji wa haki za binadamu na kutaka UNESCO isikubali kumpa tuzo kama hiyo.