Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama laelezwa kuhusu changamoto na matumaini kwa nchi ya Somalia

Baraza la usalama laelezwa kuhusu changamoto na matumaini kwa nchi ya Somalia

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limejadili hali ya usalama na machafuko yanayoendelea nchini Somalia.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Dr Augustine Mahiga, kamishna wa muungano wa Afrika kwa ajili ya amani na usalama Ramante Lamamra na mkuu wa vikosi vya muungano wa Afrika Somalia AMISOM meja jenerali Nathan Mugisha, Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameliambia baraza hilo kwamba hali ya Somalia bado ni tete lakini kuna ishara ya matumaini.

Amesema licha ya mgawanyiko wa hivi karibuni ndani ya serikali ya mpito ya Somalia, serikali hiyo imejidhatiti kuleta maridhiano na amani. Rais amemteua waziri mkuu mpya na sasa serikali ya mpito inaanzisha taasisi yake ya usalama, inawakabili wanamgambo na imeweza kuchukua tena baadhi ya miji iliyokuwa ikidhibitiwa na wanamgambo.

Lakini amesema wakati huohuo vikwazo bado vipo na vinajulikana, watu milioni mbili wanahitaji msaada wakiwemo milioni 1.4 ambao ni wakimbizi wa ndani tangu 2007 na vita vinavyoendelea vinavutia magaidi toka nje.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)