Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahabusu nchini Ugiriki ziko katika hali mbaya:Nowak

Mahabusu nchini Ugiriki ziko katika hali mbaya:Nowak

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya utesaji Manfred Nowak leo ameonya kwamba magereza nchini Ugiriki zimefurika kupita kiasi na kuwaweka katika hali mbaya maafisa wa polisi wanaokabiliana na mahamiaji wanaoingia nchini humo kupitia Uturuki kila siku.

Amesema idadi kubwa ya wahamiaji imevifanya vituo vya mpakani, vituo vya polisi na mahabusu za wahamiaji kuwa katika hali mbaya. Bwana Nowak ambaye amekuwa ziarani Ugiriki kwa wiki moja amesema anaamini serikali ya nchi hiyo ina ari ya kushughulikia changamoto hiyo, na amesema kitu muhimu kitakuwa ni kutekeleza sera mpya na mipango iliyowekwa katika wakati huu wa mdororo wa uchumi.

Ameongeza kuwa Ugiriki usibebe mzigo wote wa wahamiaji wanaoingia Muungano wa Ulaya kwani hilo ni tatizo la Ulaya yote ambalo linahitaji suluhisho la pamoja na Muungano wa Ulaya. Nowak aliyepata fursa ya kutembelea magereza na mahabusu bila taarifa amewahoji mahabusu na kubaini kwamba wengine wanashikiliwa hadi miezi sita kwenye mahabusu hizo zilizo katika hali mbaya sana, na uwezekano wa kupata huduma za afya, mawakili na wakalimani ni mdogo pia.