Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkapa aonyesha wasiwasi wake kuelekea upigaji kura ya maoni Sudan Kusini

Mkapa aonyesha wasiwasi wake kuelekea upigaji kura ya maoni Sudan Kusini

Timu maalumu iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa upigaji wa kura za maoni eneo la Sudan Kusini imeanza kuingiwa na wasiwasi juu ya hatua ndogo zinazopigwa kabla ya kufikia siku ya upigaji kura.

Timu hiyo inayoundwa na watu watatu chini ya uongozi wa rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa imesema kuwa wakati imesalia miezi mitatu tu ili upigaji kura huo ufanyike, lakini hadi sasa baadhi ya mambo muhimu ili kufanikisha uchaguzi huo bado kufanyika.

Eneo hilo la Sudan Kusini litapiga kura January 9 kuamua ama iendelea kubaki kwenye himaya ya Sudan au ijiundie taifa lake jipya.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara ya kutembelea eneo hilo, Kiongozi wa jopo hilo, Bwana Mkapa amesema kuwa kuna maaeneo muhimu bado yanaendelea kususua. Ametaja eneo mojawapo kuwa ni kutokuwepo kwa daftari la wapiga kura na kuonyesha wasiwasi kutokana na kuchelewa kukamilishwa kwa kipengele hicho.

Kuhusu jimbo lenye utajiri wa mafuta jimbo la Abyei ambalo nalo litapiga kura, Bwana Mkapa amesema kuwa hali jumla kwenye eneo hilo siyo nzuri sana lakini akaongeza kwamba kuna uwezekano wa kupiga hatua.

Hata hivyo, Makamu wa Rais wa Sudan Salva Kiir ameliambia jopo hilo kuwa kazi ya kuzikwamua changamoto inayoikabili nchi hiyo haiwezi kutatutuliwa kwa siku moja tu.