Kongamano la maendeleo Afrika lakunja jamvi Addis

Kongamano la maendeleo Afrika lakunja jamvi Addis

Viongozi wa Afrika wamehitimisha wiki nzima ya kongamano kwa ajili ya maendeo lililokuwa likifanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kongamano hilo la saba lililoandaliwa kwa ushirikiano wa tume ya maendeleo barani Afrika, muungano wa Afrika na tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi kwa ajili ya Afrika ECA. Kongamano hilo limejadili masuala mbalimbali ikiwemo ajira, kilimo, kuwawezesha wanawake na mabadiliko ya hali ya hewa.

Viongozi hao ambao wamekusanyika pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo, wataalamu wa kilimo na jumuiya za kijamii wamesema inawezekana kukabili mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa nchi tajiri zitakuwa msitari wa mbele kulisaidia bara la Afrika.

Abdoullie Janneh mkuu wa ECA amesema viongozi wa Afrika wanaona mabadiliko ya hali ya hewa kama ni changamoto kubwa kabisa ya maendeleo ya bara hilo, kwani japo hawana mchango mkubwa katika hali hiyo lakini ndio waathirika wakubwa.