Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waongeza vikwazo kwa miezi sita zaidi Ivory Coast

UM waongeza vikwazo kwa miezi sita zaidi Ivory Coast

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likitangaza kwamba Ivory Coast bado ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa, limeongeza miezi sita ya vikwazo vyake kwa taifa hilo.

Vikwazo hivyo vitakavyoendelea hadi Aprili 2011 ni vya silaha, fedha na usafiri katika nchi ambayo imegawika mapande mawili Kaskazini eneo linalodhibitiwa na waasi na Kusini linalodhibitiwa na serikali tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002.

Bila kupingwa wajumbe wote 15 wa baraza ambao mwaka jana waliongeza vikwazo kwa mwaka mmoja , wamepitisha vikwazo vya leo kwa miezi sita na kusema watatathimini hatua hiyo katika miezi miatatu ijayo baada ya uchaguzi uliocheleweshwa sana ambao sasa unafanyika tarehe 31 mwezi huu na duru ya pili itafanyika tarehe 28 Novemba kama hakutokuwa na mshindi wa moja kwa moja.

Leo ndio kampeni zinaanza rasmi na jana mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon nchini Ivory Coast bwana Y.j Choi ametoa wito kwa pande zote kuepuka ghasia zozote katika mchakato huo wa uchaguzo uliosubiriwa sana. Uchaguzi huo ilikuwa ufanyike mwaka 2005 lakini umekuwa ukiahirishwa mara kadhaa.