Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yataka eneo la amani litakalosimamiwa na UM

Sudan Kusini yataka eneo la amani litakalosimamiwa na UM

Sudan Kusini inapendekeza kuwe na eneo la amani kati ya Sudani Kaskazini na Kusini litakalosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Hayo yameelezwa na balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Bi Susan Rice alipowasilisha taarifa kuhusu ujumbe wa baraza la usalama kuzuru Sudan ambapo nchi hiyo inajiandaa kwa kura ya maoni itakayoamua hatma ya Sudan Kusini kujitenga ama la na jimbo lenye utajiri wa mafuta la Abyei litakuwa upande gani, Kaskazini ama Kusini.

Balozi Rice amesema Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameelezea hofu yake kwamba Kaskazini huenda wakawa wanajiandaa kwa vita na kusogeza vikosi upande wa Kusini.

Amesema Sudan Kusini inapendekeza eneo la amani litakalosimamiwa na Umoja wa Mataifa na liwe mili kumi kati ya mpaka wa Kaskazini na Kusini eneo ambalo hakuna majeshi yatakayoruhusiwa kuwepo

Rais Kiir pia ameelezea wasiwawsi kuhusu suala la mipaka ambalo halijatatuliwa na kusema linachelewesha maandalizi ya kura ya maoni ya Abyei na mchakato wa kura ya maoni na majadiliano ya masuala ya baada ya kura ya maoni kama kugawana mafuta na utajiri wa nchi.