Waliokuwa wanajeshi watoto wasaidiwe kurejea maisha ya kawaida:UM

13 Oktoba 2010

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa anayeendesha mikakati ya kumaliza kuajiriwa kwa watoto jeshini ametoa wito kwa serikali kutoa usaidizi unaohitajika kuhakikisha watoto hao wanarejea maisha yao ya kawaida wanapoachiliwa kutoka jeshini.

Mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya ya watoto na mizozo Radhika Coomaraswamy amesema ikiwa watoto hao hawatasaidiwa kurejea maisha ya kawaida ni rahisi sana wao kuingia kwenye makundi ya uhalifu au kuwa watoto wa kurandaranda mitaani.

Akiongea na waandishi wa habari kabla ya kuwasilisha ripoti mpya kuhusu suala hilo kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa anasema kuwa changamoto kubwa iliyo sasa ni ukosefu wa mpango wa kuwasaidia watoto waliotoka jeshini.

Ripoti hiyo inaonyesha kati ya mafanikio mwaka uliopita ambapo watoto wanajeshi 3000 waliachiliwa kutoka kwa kundi la Mao nchini Nepal , mipango ya kuachiliwa kwa watoto 900 kutoka kwa waasi wa SPLM nchini Sudan itimiapo mwezi Novemba na kuachiliwa kwa watoto wote kutoka kwa waasi wa FNLnchini Burundi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter