Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa UM wa kura ya maoni Sudan wajadili usalama

Ujumbe wa UM wa kura ya maoni Sudan wajadili usalama

Jopo la waangalizi wa Umoja wa Mataifa linalofuatilia kura ya maoni ya Sudan Kusini limekutana na viongozi wa eneo hilo kujadili hali ya usalama na maandalizi kwa ujumla.

Kura hiyo ya amani iliyopangwa kufanyika Januari 9 mwakani itaamua mustakabali wa mamilioni ya watu wa Sudan, na pia kushudia endapo kura hiyo itaamua Sudan Kusini ijitenge kutoka milki ya Sudan na kuwa taifa huru. George Njogopa na taarifa kamili.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Likiwa kwenye ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali,jopo hilo ambalo liliundwa na Katibu Mkuu Ban Ki-moon likiongozwa na aliyewahi kuwa rais wa Tanzania Benjamin Mkapa limekuwa na majadiliano ya kina na Kiongozi wa eneo hilo ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Sudan Salva Kiir,huko Juba ambako ni makao makuu ya eneo hilo.

Baada ya majadiliano hayo, Kiongozi wa jopo hilo Bwana Mkapa aliwaambia waandishi wa habari masuala muhimu yaliyopewa uzito ikiwemo haja ya kuwepo kwa upigaji kura katika mazingira ya haki na ukweli. Mkapa amesema kuwa yeye bado anamatumaini kuwa kura hiyo ya maoni itafanyika kwa amini kama ilivyopangwa Januaru 9.