Kukabiliana na majanga ni jukumu la kila mtu:Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amesema miji kote duniani hivi sasa iko katika hatari kubwa ya majanga kuliko wakati mwingine wowote na kuna haja ya juhudi za kimataifa kuhakikisha miji hiyo imeboreshwa.
Katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupunguza majanga Ban amesema maneno kama kubwa sana, la mauaji, na baya kuwahi kutokea yamekuwa yakigonga vichwa vya habari mwaka huu kutokana na mafuriko, matetemeko na vimbunga, na amesema maneno haya yataendelea kusikika kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la majanga hayo.
Ameongeza kuwa kwa kulitambua hilo sasa kazi ya kupunguza majanga ni jukumu la kila mtu, kuanzia serikali, mashirika ya kimataifa, jumuiya za kijamii na watu binafsi ili kuweza kuokoa maisha ya maelfu ya watu yanayopotea wakati majanga yanapozuka.