Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miji inatakiwa kuchukua hatua kujiandaa na majanga ya asili:UM

Miji inatakiwa kuchukua hatua kujiandaa na majanga ya asili:UM

Leo ni siku ya kimataifa ya kupunguza majanga ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 13. Karibu watu milioni 256 duniani kote wameathirika na majanga ya asili kama tetemeko la ardhi, mafuriko, kimbunga na maporomoko ya ardhi.

Kwa mujibu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa cha mikakati ya kupunguza majanga duniani ISDR majanga hayo yamekatili maisha ya watu 236,000, na asilimia 90 ya wanaoathirika wanaishi katika miji. ISDR imetoa wito kwa serikali kuifanya miji yao kuwa salama dhidi ya majanga.

Margareta Wahlstrom ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu katika upunguzaji wa hatari ya majanga, anasema mipango ya miji mibaya inawaweka mamilioni ya watu katika hatari ya majanga ambayo ingeweza kuepukika.

(SAUTI MARGARETA WAHLSTOM)

Nalo shirika la afya duniani WHO katika kuadhimisha siku hii limetoa wito kwa serikali na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa imara kuhimili matetemeko ya ardhi, mafuriko, vimbunga na majanga mengine.

Shirika hilo limesema uharibifu wa mamia ya hospitali na vituo vya afya katika mafuriko ya Pakistan, tetemeko la Haiti na majanga mengine vinadhihirisha tishio linalokabili huduma za afya katika miji duniani kote na haja ya kulipa uzito.

Kufikia Septemba mwaka huu majanga ya asili kote duniani yanakadiriwa kusababisha uharibufu wa dola bilioni 81.