Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwalinda watoto katika majanga ni muhimu:UNICEF

Kuwalinda watoto katika majanga ni muhimu:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa wito wa kuongeza juhudi za kimataifa za hatua za kupunguza athari wakati wa majanga na kuwalinda watoto.

Wito huo umetolewa katika mkesha wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupunguza hatari za majanga ambayo kila mwaka huadhimishwa Oktoba 13. UNICEF inasema watoto huwakilisha asilimia 50 hadi 60 ya wanaoathirika wakati wa majanga, iwe ni katika kupoteza maisha au maradhi yanayosababishwa na utapia mlo, maji na usafi, ambayo huongezeka wakati majanga ya asili yanapotokea .

Kwa mujibu wa UNICEF athari hizo za majanga kwa watoto ni pamoja na kuingilia pia mfumo wa elimu, kuwaathiri kiakili, kuchangia watoto hao kunyanyasika, kunyonywa na hata kutumikishwa kutokana na hali inayowakabili.