Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yaathiri maelfu ya watu Afrika Magharibi:OCHA

Mafuriko yaathiri maelfu ya watu Afrika Magharibi:OCHA

Shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA linasema zaidi ya watu milioni moja wameathirika na mafuriko Afrika ya Magharibi.

Shirika hilo linasema hadi sasa watu zaidi ya 400 wamefariki dunia, nyumba kubomolewa, miundombunu kuathirika vibaya na watu kupoteza mali na mifugo yao. Nchi kumi zimekumbwa na mafuriko hayo na Benin ndio iliyoathirika vibya Zaidi., zingine ni Nigeria, Niger, Chad, Sudan, Cameroon, Mauritania, Gambia, Burkina Faso, Guinea na Ghana. George Njogopa na taarifa zaidi

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA limesema kuwa zaidi ya watu milioni 1.7 wameathiriwa na mafuriko katika eneo la Afrika Magharibi. Mafuriko hayo pia yamesababisha watu 421 kupoteza maisha wakati Benin ndiyo iliyoathiriwa vibaya zaidi kwani idadi jumla waliathiriwa inafikia 641,137 na wengine 86 wakipoteza maisha. Nigeria inafuatia ikiwa na waathiriwa zaidi 300,000 wakati waliopoteza maisha wanafikia 118.

Kuna wasiwasi mkubwa wa kuanza kuripuka kwa magonjwa ya kuhara, na tayari Shirika hilo la Umoja wa Mataifa OCHA limesema linataarifa ya kuanza kuripuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika nchi za Nigeria, Chad, Cameroon na Niger. Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP limetoa kiasi cha dola 185,000 ili kufadhilia shughuli za kukabiliana na mafuriko hayo nchini Benin.