Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kundi la kufuatilia kura ya maoni Sudan lafanya ziara yake ya kwanza Sudan

Kundi la kufuatilia kura ya maoni Sudan lafanya ziara yake ya kwanza Sudan

Wanachama wa jopo la Umoja wa Mataifa waliotwikwa jukumu la kufuatilia kura ya maoni itakayoandaliwa nchini Sudan wameanza ziara yao ya kwanza nchini humo.

Wanachama hao waliwasili mji mkuu wa Sudan Khartoum mwishoni mwa wiki kwa ziara ya juma moja ambapo watazuru mji mkuu wa Sudan kusini Juba na Abyei. Januari mwakani wenyeji wa Sudan Kusini watapiga kura ya kuamua iwapo watajitenga na sehemu zingine za nchi huku wenyeji wa Abyei ambalo ni eneo lililo kati kati mwa nchini nao wakipiga kura ya kuamua iwapo watajiunga na eneo la kaskazini au kusini. Kura hiyo ya maoni itakuwa awamu ya mwisho ya kutekelezwa kwa makubalino ya makataba wa amani uliotiwa sahihi mwaka 2005 kumaliza vita vilivyodumu kwa miongo miwili kati ya serikali ya kaskazini mwa Sudan na jeshi la Sudan People's Liberation Movement SPLM lililo kusini. Kamati hiyo ambayo inawajumuisha aliyekuwa rais wa Tanzania Benjamin Mkapa, aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Ureno António Monteiro na aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Nepal Bhojraj Pokharel itafanya mikutano na maafisa kutoka serikali ya Sudan , kutoka serikalia ya kusini mwa Sudan , tume inayohusika na kura hiyo kusini mwa sudan , waakilishi wa Umoja wa Mataifa , makundi ya waangalizi na waakilishi wa mashirika ya umma.