Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wataka kura ya maoni Sudan kufanyika kwa amani

UM wataka kura ya maoni Sudan kufanyika kwa amani

Ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa unaozuru Sudan umesema kuwa ni lazima kura ya maoni inayotarajiwa kuandaliwa nchini humo Januari mwakani ifanyike wakati ufaao na kwa njia ya amani kulingana na makubalino ya amani yaliyomaliza vita kati ya Sudan Kusini na kaskazini.

Ujumbe huo unaoongozwa na balozi Susan Rice unasema kuwa baraza hilo linaunga mkono shughuli hiyo. Januari mwakani wenyeji wa kusini mwa Sudan watapiga kura ya kuamua iwapo watajitenga na sehemu zingine za nchi huku wenyeji wa eneo lililo kati kati mwa Sudan la Abyei wakipiga kura ya kuamua iwapo watajiunga na kaskazini au kusini.

Kura hiyo ya maoni itakuwa awamu ya mwisho ya kutekelezwa kwa makubalino ya CPA yaliyotiwa sahihi mwaka 2005 kumaliza mapigano ya miongo miwili kati ya serikali ya kaskazini na wapiganaji wa kundi la SPLM lililo kusini.

Ziara hiyo inajiri baada ya mkutano kuhusu Sudan uliondaliwa mjini New York na kutoa wito kwa jamiii ya kimataifa kuheshimu matokeo yoyote ya kura hiyo ya maoni ikiwa itaandaliwa kwa njia inayofaa.