Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa kimataifa pekee ndio utatatua tatizo la usafirishaji haramu wa watu UM

Ushirikiano wa kimataifa pekee ndio utatatua tatizo la usafirishaji haramu wa watu UM

Kwa mara ya kwanza wataalamu wa kupinga usafirishaji haramu wa watu kutoka mashirika mbalimbali ya kikanda wamekutana Dakar Senegal katika mpango ulioanzishwa na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu usafirishaji haramu wa watu, hususan wanawake na watoto.

Mwakilishi huyo Joy Ngozi Ezeilo amesema mkutano wao uliomalizika jana umejadili ni jinsi gani mashirika hayo yanavyoweza kufanya kazi pamoja na mfumo wa Umoja wa Mataifa hasa katika kupashana habari ili kukomesha tatizo hilo.

Joy amesema ushirikiano ni muhimu sana katika kumaliza tatizo hili ambaolo limekwisha athiri mamilioni ya watu. Jason Nyakundi na taarifa zaidi.

(RIPOTI YA JAYSON NYAKUNDI)

Bibi Ezeilo amesema kuwa ushirikiano kati ya pande zinazohusika kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu unahitajika ili kukabiliana na uovu huo. Wataalamu kutoka Afrika , Amerika , Asia , Ulaya na Mashariki ya kati walijadili masuala yanayohusiana na uzuiaji wa usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na usalama kwa wanaosafirishwa.

Ezeilo amesema kuwa masuala ya kuwasaidia na kuwalinda wanaosafirishwa kiharamu yanastahili kutolewa bila masharti yakiwemo pia masuala ya kulinda haki zao. Ameongeza kuwa mashirika yanayopambana na usafirishaji huo haramu wa binagamu yanastahili kuhakikisha kuwa sera zao zinaambatana na haki za binadamu na kuangazia zaidi umri na jinsia.