Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja ni silaha ya kukabili changamoto za dunia:Ban

Umoja ni silaha ya kukabili changamoto za dunia:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuwa ushirikiano wa kimataifa ndiyo suluu pekee inayoweza kuzikabili changamoto za dunia ikiwemo vitendo vya kigaidi, matatizo ya njaa, uhalifu wa kupangilia na mabadiliko ya tabia nchi.

Akiwahutubia wajumbe wa ngazi ya juu wanaohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa unaohusika na madawa ya kulevya na uhalifu,mkutano ambao umefunguliwa kwa niaba yake ya Mkurugenzi Mkuu ofisi ya Umoja wa Mataifa wa kudhibiti madawa ya kulevya na uhalifu Yury Fedotov, amesema kuwa hakuna taifa linaloweza kupiga hatua kuzitatua changamoto hizo bila kuwepo ushirikiano na taifa jingine.

Mkutano huo unafanyika Sochi, nchini Russia . Amesema ulimwengu wa sasa ni wenye mafungamano na mashabiano makubwa,hivyo ni rahisi kuzikabili changamoto hizo kwa kusaka nguvu ya pamoja tena kwa weledi na ustadi mkubwa.

Hata hivyo ameipongeza Russia iliyo mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa kuandaa mkutano huo katika eneo la Sochi sehemu ambayo inatazamiwa pia kuwa mwenyeji wa michuano ya Olimpiki ya majira ya baridi.