Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani mauaji ya mpiga picha wa TV nchini Iraq

UNESCO yalaani mauaji ya mpiga picha wa TV nchini Iraq

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Irina Bokova leo amelaani vikali mauaji ya mpiga picha wa televisheni wa Iraq aliyeuawa kwenye bomu lililotegwa kwenye gari nje ya mji wa Baghdad.

Tahrir Kadhim Jawad mwenye umri wa miaka 27 alikuwa akiendesha gari lake kuelekea mjini Baghdad wakati bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari lake lilipolipuka kwenye mji wa Garma jimbo la Anbar.

Kwa mujibu wa Bokova Jawad alikuwa mwandishi wa habari kwa miaka saba, kwanza kama mhariri wa gazeti la kila wiki nchini humo Al-Karma na kisha kuwa mpiga picha wa kujitegemea kwa televisheni mbalimbali.

 Bokova amesema mwandishi huyo amepoteza maisha akiwajibika kwa jina la uhuru wa kujieleza ambao ni haki ya binadamu kwa jamii yoyote ya kidemokrasia. Kwa mujibu wa kamati isiyo ya kiserikali ya kuwalinda waandishi habari Bwana Jawad ni mwandishi wa tatu kuuawa nchini Iraq katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja .