Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF imetoa msaada mkubwa kwa Pakistan na Afrika Magharibi

CERF imetoa msaada mkubwa kwa Pakistan na Afrika Magharibi

Mashirika ya misaada ya kibinadamu kukabiliana na msaada wa dharura Pakistan, Niger na Chad ndio yaliyopokea msaada mkubwa kutoka kitengo cha fedha za dharura cha Umoja wa Mataifa CERF.

Fedha hizo ni zile zilizotolewa na CERF katika robo ya tatu ya mwaka huu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA, CERF ambayo hutoa fedha haraka kuwasaidia watu walioathirika na majanga na vita ilitoa karibu dola milioni 40 kwa mashirika ya misaada yanayotoa huduma kuokoa maisha mamilioni ya walioathirika na mafuriko Pakstan .

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita shirika la mpango wa chakula duniani WFP limepokea jumla ya dola milioni 15 kukabiliana na matatizo ya chakula Niger ambayo yamewaacha watu milioni 7 wakihitaji msaada wa dharura wa chakula. Na kuanzia mwanzo wa mwaka huu mashirika ya misaada nchini Niger yamepewa dola milioni 35 na CERF.

Dola zingine zaidi ya milioni 10 zimekwenda kwa mashirika ya misaada nchini Chad ambako yanasaidia kukabiliana na matatizo ya utapia mlo yaliyosababishwa na upungufu wa chakula. Mashirika mengi ya misaada ya dharura yaliyopata msaada kutoka kwa CERF ni Myanmar dola milioni 6.4 kusaidia waathirika

wa mafuriko na maporomoko ya ardhi kwa ajili ya kuwapa waathirika chakula, malazi, maji na vifaa vya usafi.

Burkina faso imepata msaada wa dola milioni 2 kuwasaidia watu zaidi ya 105,000 walioathirika na mafuriko. Mashirika kama UNICEF na WHO yamepewa dola milioni 2 ili kusaidia matatizo ya afya na watoto nchini Nigeria. Madagascar ilipewa dola milioni 4.7 kupambana na nzige huku Georgia ikipokea dola 293,000 pia kupambana na nzige.

Mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa luliunda CERF mwaka 2005 ili kutoa msaada kwa waathirika wa majanga na matatizo mengine ya kibinadamu yanayohitaji fedha za dharura.