Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau wa maendeleo wanataka Global Fund itunishwe ili kufikia malengo ya milenia

Wadau wa maendeleo wanataka Global Fund itunishwe ili kufikia malengo ya milenia

Jumuiya ya kimataifa ambayo ni wadau wa kupigia chepuo malengo ya maendeleo ya milenia wametoa wito wa kutunisha mfuko wa kimataifa yaani Global Fund ili kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria.

Wadau hao ambao wanakutana tangu jana wanasema hii ni fursa muhimu ya kuendelea kupiga hatua katika kufikia malengo ya milenia. Mfuko wa kimataifa umekuwa ni moja ya washirika muhimu na waliofanikiwa katika vita dhidi ya maradhi hayo matatu yanayokatili maisha ya watu wengi katika nchi masikini.

Nchi 144 duniani zinafaidika na mfuko huo ambao unategemea fedha kutoka kwa wahisani kusaidia mipango ya kitaifa na kuchagiza ushirikiano kati ya sekta za umma, sekta binafsi na jumuiya za kijamii, na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa kutoa kinga, chanjo na tiba.

Mafanikio ya mfuko huo ni muhimu katika kufikia malengo ya milenia na kwa sasa Global Fund inasema inahitaji dola bilioni 17 katika miaka mitatu ijayo kuanzia 2011-2013 na kuweza kufikia malengo hayo inahitaji dola bilioni 20.