Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pongezi vijana kwa kutaka kutokomeza silaha za nyuklia:Ban

Pongezi vijana kwa kutaka kutokomeza silaha za nyuklia:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amepongeza jitihada za jumuiya za kijamii zenye lengo la kuchagiza kuhusu umuhimu wa kupunguza gharama za matumizi ya kijeshi na kuweza kuwa na dunia huru bila silaha za nyuklia.

Akizungumza kwenye mkutano wa dini kwa ajili ya amani mjini New York Ban amesema mpango huu muhimu kutoka kwa vijana zaidi ya milioni tano wa dini na imani mbalimbali ni ishara tosha ya jumuiya za kijamii kuunga mkono vita vya kutokomeza nyuklia. Ban amesema gharama za matumizi ya kijeshi duniani zimeongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka 2000 na kufikia zaidi ya trilioni 1.5.

Na amesema fedha hizo ingekuwa bora zikatumika kupunguza umasikini, mabadiliko ya hali ya hewa , kununua chakula na lishe bora kwa jamii, kwa afya ya kina mama na watoto na kukabili changamoto zingine za maendeleo. Pia amekaribisha mchango wa kundi la kampeni la vijana Arms Down Global Youth campaign for shared security ambalo limekuwa likichagiza na kuelimisha watu juu ya umuhimu wa kupunguza bajeti za matumizi ya kijeshi na kupigia upatu kuwa na dunia huru bila silaha za nyuklia.

Kuongeza kasi ya kutokomeza silaha za nyuklia imekuwa ni moja ya mambo yanayopewa kipaumbele na Katibu Mkuu tangu mwaka 2007 alipoingia madarakani. 2008 Ban aliwasilisha mpango wa kupokonya silaha za nyuklia na kutozizalisha kwa wito wa pande zote kutia saini mkataba wa masuala ya nyuklia NTP na kufanya majadiliano kuhusu kuachana na silaha hizo na kuwa na mkataba mpya.