Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zinahitajika kukabili mabadiliko ya hali ya hewa:Figueres

Juhudi zinahitajika kukabili mabadiliko ya hali ya hewa:Figueres

Katibu mkuu mtendaji wa mpango wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa UNFCCC Christiana Figueres amezitolea wito serikali kuongeza juhudi za kufikia muafaka wa kuchukua hatua muhimu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Wito huo umetolewa leo mjini Tianjin Uchina ambako serikali mbalimbali zinakutana kwenye mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Ikiwa imesalia chini ya miezi miwili kabla ya mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa Canun Mexico, Bi Figueres amesema matokeo muhimu yanahitajika sana mwezi Desemba ili kurejesha imani katika uwezo wa pande zote kusukuma mbele mjadala huo. Jason Nyakundi na taarifa zaidi

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Ikiwa imesalia chini ya miezi miwili kabla ya kuandaliwa kwa mkutano wa Umoja wa Matiafa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa mjini Cancun nchini Mexico bibi Figueres amesema kuwa matokeo mazuri ya mkutano wa Disemba yanahitajika.

Amesema kuwa mataifa mengi yameweka matumaini yao kwenye mkutano huo akiongeza kuwa ni lazima yahakikishe kuwa ulimwengu wote umeamini kuendelea kujitolea kwa kila nchi siku zijazo kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema kuwa masuala yakiwemo kupeleka teknolojia isiyochafua mazingira kwa nchi zinazoendelea na kuchangisha fedha za kugharamia masuala ya hali ya hewa kwa nchi hizo ni baadhi ya makubaliano yanayohitajika. Hata hivyo amesema kuna sehemu zinazosababisha kuwepo kwa tofauti zikiwemo za kuafikia jinsi ya kugawana majukumu ya mabadiliko ya hali ya hewa ya sasa hivi na ya siku zijazo.