Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya kimataifa ya makazi: miji bora, maisha bora

Leo ni siku ya kimataifa ya makazi: miji bora, maisha bora

Leo ni siku ya kimataifa ya makazi na mwaka huu kauli mbiu ni miji bora , maisha bora, ujumbe unaokwenda sawia na ule wa maonesho ya dunia ya Shangai, yaani Shangai World Expo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT katika kuadhimisha siku hii ambayo kimataifa inafanyika mjini Shangai imewaalika waandishi wa habari na watu wanaojali maendeleo ili kuchagiza kuhusu hali ya miji na haki ya kila mtu kuwa na makazi.

Mbali ya Shangai hafla za kuadhimisha siku hii pia zinafanyika Nakuru Kenya, Barcelona Hispania na Kolkata India. Katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha sikuu hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameelezea ukweli kwamba watu bilioni moja wanaoishi kwenye mitaa ya mabada na nyumba zisizo na viwango vinavyostahili wengi wako katika nchi zinazoendelea, hawana uwezo na wengi wao wako chini ya miaka 25.

Ameongeza kuwa masikini wanaoishi mijini mara nyingi hawana huduma muhimu na wanaishi kwa matumaini ya kupata elimu na kazi nzuri. Amesema changamoto za mijini kama uharibifu wa mazingira, uhalifu vinahitaji suluhu ya pamoja ili kujenga miji bora na maisha bora kuanzia kwa serikali, jumuiya za kijamii, sekta binafsi na msaada wa mfumo wa Umoja wa Mataifa.