Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathirika wa mafuriko Pakistan wanarejea makwao:OCHA

Waathirika wa mafuriko Pakistan wanarejea makwao:OCHA

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA leo limesema idadi kubwa ya watu waliosambaratishwa na mafuriko nchini Pakistan ama wamerejea katika maeneo yao ya awali au wanafanya hivyo.

OCHA inasema mafuriko hayo yaliwaathiri watu zaidi ya milioni 20 ambao ni takrikabi asilimia 10 ya watu wote huku asilimia 75 wakitoka jimbo la Sindh na Punjab.

Shirika hilo linasema hata hivyo wengi wanarejea katika mjimbo mengine lakini sio Sindh jimbo ambalo liliathirika zaidi na mafuriko hayo.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaongeza msaada kwa waathirika wa mafuriko hayo ambayo yalikatili maisha ya watu wapatao 2000 na kuwaacha mamilioni bila makazi, wakiwa na utapia mlo, hatari ya maradhi na kupoteza mali na mifugo yao.

Hadi sasa shirika la afya duniani WHO limeshatoa msaada wa madawa kwa watu karibu milioni 5 na kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wametoa vyandarua 500,000 vyenye dawa kama hatua ya kwanza ya kukabiliana na ongezeko la malaria. Familia zaidi ya 448,400 zimepata mahema na vifaa vingine vya malazi huku watu milioni 3.6 wanapata maji safi ya kunywa, na msaada wa chakula unatolewa kwa watu milioni saba.