Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yatoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Charpak

UNESCO yatoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Charpak

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO ameelezea huzuni yake kufuatia kifo cha mwanasayansi wa Ufaransa Georges Charpak ambaye alikuwa mshindi wa tuzo ya nobel ya fizikia mwaka 1992.

Bwana Charpak ambaye amefariki dunia jana mjini Paris akiwa na umri wa miaka 86 alikuwa pia mwanzilishi wa jumuiya iliyokuwa na lengo la kuanzisha elimu ya sayansi kwenye shule za msingi nchini Ufaransa. Irina Bokova amesema kwa kifo cha Charpak, UNESCO imepoteza mtaalamu ambaye mchango wake katika ushirikiano wa sayansi duniani bado una uzito mkubwa katika maeneo mengi ya kazi za shirika hilo.

Amesema Georges hakuwa tuu mwana sayansi mzuri bali pia muungaji mkono mkubwa wa maadili na mawazo ya UNESCO, alikuwa msisimuaji mkubwa katika mkutano wa 2005 wa kuzindua mwaka wa kimataifa wa fizikia. Charpak alizaliwa mwaka 1924 katika kitongoji cha Wayahudi mashariki mwa Poland , na alipata uraia wa Ufaransa mwaka 1946.