Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pakistan lazima ikabiliane na ugaidi asema afisa wa India:

Pakistan lazima ikabiliane na ugaidi asema afisa wa India:

Waziri wa mambo ya nje wa India ametoa wito kwa Pakistan kutekeleza wajibu wake wa kutoruhusu himaya yake kutumiwa na ugaidi dhidi ya India.

Akizungumza kwenye mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa S.M Krishna amesema Jammu na Kashmir ambayo ni sehemu ya India ni mlengwa wa ugaidi na wanamgambo wanaofadhiliwa na Pakistan. Jimbo la Kashmir liligawika mapande mawili upande kwa India na mwingine kwa Pakistan baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1947.

Kundi la kijeshi la uangalizi la Umoja wa Mataifa kwa nchi hizo mbili UNMOGIP lilipelekwa kwa ajili ya kuhakikisha mapigano yanasitishwa Jammu na Kashmir tangu mwaka 1949. Waziri huo amesema kama majirani mataifa hayo mawili yana jukumu la kufanya kazi pamoja kutokomeza ugaidi.

Jana waziri wa mambo ya nje wa Pakistan aliuambia mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake iko tayari kwa mazungumzo na India ili kupata suluhu ya mzozo wa jimbo la Kashmir ambao amesema ni moja ya mizozo ya muda mrefu katika ajenda za Umoja wa Mataifa.