Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa uchaguzi nchini Afghanistan upewe muda zaidi:UM

Mchakato wa uchaguzi nchini Afghanistan upewe muda zaidi:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Staffan de Mistura amesema ni mapema mno kutoa hukumu dhidi ya uchaguzi wa karibuni uliofanyika nchini humo.

Akiliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu hali ya Afghanistan amesema ukizingatia kwamba uchaguzi umefanyika Septemba 18 katika nchi ambayo bado ina machafuko ni hatua muhimu sana iliyofikiwa na nchi hiyo. Ameongeza kuwa licha ya visa vya machafuko, zaidi ya watu milioni nne walijitokeza kupiga kura, na asilimia 37 ya wapiga kura walikuwa wanawake.

De Mistura ameliambia Baraza la Usalama ni mapema kutoa kauli ya mwisho kuhusu mchakato wa uchaguzi huo. Amesema turuhusu muda zaidi kabla ya kutoa hukumu. Tuzingatie uchaguzi wa mwaka jana ambao ulitoa somo pia kwa Umoja wa Mataifa la kuwa makini kutoa maazimio , tuwe makini na kutoa msaada zaidi kwa ajili ya watu wa Afghanistan.

Ameongeza kuwa baada ya mchakato mzima wa uchaguzi kukamilika kutakuwa na mjadala kuhusu mipango ya muda mrefu ya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.