Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sierra Leone yakaribisha hatua ya kuondolewa vikwazo:

Sierra Leone yakaribisha hatua ya kuondolewa vikwazo:

Sierra Leone imekaribisha hatua ya kuondolewa vikwazo ilivyokuwa imewekewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1990.

Uingereza ambayo ilikuwa msitari wa mbele kutaka vikwazo hivyo imechagiza vitolewe ikisema havihitajiki tena. Balozi wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa Shekou Touray amesema hatua hiyo ni ishara muhimu kwamba nchi hiyo inaelekea kunakostahili.

Amesema ingawa bila shaka bado kuna masuala ya kuyapatia ufumbuzi anadhani kwamba sasa kutakuwa na biashara huru na uingiaji wa bidhaa na masuala mengine yaliyokuwa yanakwamisha uchumi yatatatuliwa. Ameongeza kuwa pia masuala ya bima na washirika ambao walikuwa wanahofia ushirikiano na Sierra leone kwa ajili ya vikwazo watafungua mlango.

Amesema hatua hiyo ya kuondoa vikwazo itaisaidia nchi hiyo kujenga upya uchumi wake. Baraza la usalama pia limepiga kura ya bila kupingwa kuongeza muda wa mpango wake wa ujenzi wa amani Sierra Leone UNPISIL kwa mwaka mmoja zaidi hadi tarehe 15 Septemba 2011.