Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sierra Leone inahofia hali ya Guinea:Mwakilishi wa UM

Sierra Leone inahofia hali ya Guinea:Mwakilishi wa UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone Michael von der Schulenburg amesema nchi hiyo inahofia hali inayoendelea katika nchi jirani ya Guinea.

Guinea inajiandaa na uchaguzi ambao utairejesha nchi hiyo kwenye utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2008. Schulenberg ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kuhusu Sierra Leone kwenye baraza la usalama.  Ameliambia baraza hilo ambalo linajihusisha na masuala ya amani na usalama wa kimataifa kwamba yale yatakayojiri Guinea yatakuwa na athari pia Sierra Leone na Afrika ya Magharibi kwa ujumla.

Amesema endapo Guine itafanikiwa katika kipindi hiki cha mpito cha demokrasia itasaidia kanda nzima kuwa tulivu na kurahisisha kazi ya Sierra Leone katika kutatua matatizo ya kikanda. Ameongeza kuwa na endapo hali ya gueine haitakuwa kama inavyotarajiwa au mchakato mzima kubadilika hili linaweza kuwa na athari kubwa kwa Sierra leone.

Ikiwemo masuala ya mipaka, tamaduni, ukabila, uhusiano baina ya mataifa hayo mawili na silaha ndogondogo vinaweza kuleta matatizo makubwa Guinea na kuingia hadi Sierra Leone. Matatizo yanayoisumbua Afrika Magharibi hivi sasa amesema ni pamoja na biashara za mpakani, usafirishaji wa mihadarati na uvuvi haramu.