Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitika Israel kutoongeza muda wa kusitika ujenzi wa makazi ya walowezi

Ban asikitika Israel kutoongeza muda wa kusitika ujenzi wa makazi ya walowezi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amesema amesikitishwa na hatua ya Israel ya kutoongeza muda wa kusitisha ujenzi wa makazi ya walowezi kwenye eneo linalokaliwa la Wapalestina.

Ameelezea hofu yake juu ya hatua zinazochukuliwa kwenye eneo hilo. Amerejea taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na Quartet yaani Umoja wa Mataifa, muungano wa Ulaya, Urusi na Marekani ambayo ilitoa wito wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa kuitaka Israel kuongeza muda wa sera ya kuzuia ujenzi wa makazi ya walowezi.

Ban amerejea kusema shughuli zote za ujenzi wa makazi katika eneo linalokaliwa la Palestina ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa. Ameitaka Israel kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia mpango wa amani na kusitiza ujenzo wa makazi ya walowezi.

Katibu Mkuu anaunga mkono juhudi zinazofanyika za kutafuta njia ya kuendelea na na mazungumzo ya amani katika mazingira ambayo ni mazuri kwa kupiga hatua. Amesema hii ndio njia pekee itakayopelekea kuundwa kwa taifa la Palestina ambalo litaishi kwa amani na jirani zao Israel.