Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zichukuliwe dhidi ya wabakaji DR Congo:Wallstrom

Hatua zichukuliwe dhidi ya wabakaji DR Congo:Wallstrom

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa leo ametoa msukumo wa kuchukuliwa hatua viongozi wa makundi ya waasi waliohusika na ubakaji wa kundi la watu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Margot Wallstrom ambaye ni mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia ukatili wa kimapenzi kwenye maeneo ya migogoro amesema hatua za haraka zinahitajika dhidi ya wahalifu hao kabla kesi zao hazijapoa.

Ameyataja makundi hayo kuwa ni FDLR na wanamgambo wa Mai-Mai. Amesema majina hayo ni chanzo na yatasaidia kuwabaini wengine waliohusika katika ubakaji wa kundi la watu wengi nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Watu 303 walibakwa katika vijiji 13 kwenye jimbo la Walikale mkoa wa Kivu ya Kaskazini, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto. Wallstrom amesema pia chanzo cha mgogoro mashariki mwa congo lazima kipewe uzito.