Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia inahitaji msaada kama wa Iraq na Afghanistan:Mahiga

Somalia inahitaji msaada kama wa Iraq na Afghanistan:Mahiga

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia leo ametoa wito wa washirika wa kimataifa kusaidia kuleta amani, utulivu na maridhiano ya kitaifa nchini Somalia.

Balozi Augustine Mahiga amesema utahitajika msaada sio tofauti na ule uliotolewa kwa mataifa mengine ambayo yamekabiliwa na matatizo makubwa kama Somalia. Amesema wote tumeona jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyosaidia serikali za Iraq na Afghanistan, Somalia haina tofauti, inahitaji msaada kama huo.

Akizungumza kwenye mkutano mjini Madrid wa kundi la kimataifa kwa ajili ya Somalia ICG, Mahiga amesema serikali ya mpito na jumuiya ya kimataifa lazima wafanye kazi kwa karibu kama wanataka kumaliza mgogoro wa Somalia.

Ameongeza kuwa nchi haina serikali kuu tangu mwaka 1991, imesambaratishwa na miongo ya vita na hivi karibuni wanamgambo wa Kiislamu wa Al-Shabaab. Watu milioni 3.2 ikiwa ni zaidi ya asilimia 40 ya watu wote wanahitaji msaada.