Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wafanya mkutano leo kujadili hali ya Sudan

UM wafanya mkutano leo kujadili hali ya Sudan

Umoja wa Mataifa baadaye hii leo unafanya mkutano wa ngazi ya juu kujadili suala la Sudan. Wakuu wan chi na serikali kutoka kote duniani wanaohudhuria mjadala wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wataketi na uongozi wa Sudan kutoka eneo la Kaskazini na la Kusini pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kujadili masuala nyeti kuhusu kura ya maoni na mchakato wa amani ya Darfur.

Hiyo itakuwa fursa muhimu kwa viongozi wa Sudan kurejea wajibu wao wa kufanya kazi pamoja na pia kuijumuisha jumuiya ya kimataifa hasa katika wakati huu ambao ni muhimu sana katika historia ya nchi hiyo.

Kumekuwa na hofu kuhusu kura mbili za maoni zilizopangwa kufanyika nchini Sudan Januari mwakani ile ya Sudan Kusini kutaka kujitenga na ile ya eneo lenye utajiri wa mafuta la Abyei, na pia usalama wa jimbo la Darfur.