Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na Salva Kiir kujadili kura ya maoni Sudan

Ban akutana na Salva Kiir kujadili kura ya maoni Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amefanya mazungumzo na Makamu wa kwanza wa Rais Sudan Salva Kiir kuhusiana na kura ya maoni inatotazamiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao kuamua hatma ya eneo la Kusin mwa Sudan na jimbo la Kati Abyei.

Wananchi wa eneo hilo la Kusini mwa Sudan watapiga kura mwezi January mwakani kuamua kama ijiundie taifa lake na kujitenga na Sudan. Katika majadiliano hayo, Ban Ki-moon ameonyesha wasiwasi wake hasa kutokana kuchelewa kuundwa kwa kamishna maalumu itayoratibu kura hiyo ya maoni kwa upande wa Jimbo la Abyei.

Hata hivyo viongozi hao wawili wameelezea umuhimu wa kuendesha kura hiyo ya maoni kwa wakati na kuepukwa kwa vitendo vya vurugu na uvunjikaji wa amani. Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa ndiye atayeongoza jopo la waangalizi ambalo pia linawahusisha viongozi wengine kadhaa akiwemo waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ureno Antonio Monteiro.