Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zinahitajika kumuinua mwanamke kiuchumi:Bachelet

Juhudi zinahitajika kumuinua mwanamke kiuchumi:Bachelet

Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kushughulikia masuala ya wanawake kiitwacho UN-Women Michelle Bachelet amesema juhudi zinahitajika ili kuinua kiwango cha uchumi cha wanawake.

Bi Bachelet ameyasema hayo katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari mjini New York tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa chombo hicho ambacho ni muunganiko wa mashirika manne ya Umoja wa Mataifa ayanayochagiza masuala ya usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake. Bi Bachelete amesema kuwawezesha wanawake kiuchumi itakuwa na umuhimu mkubwa katika UN-Women pamoja na masuala mengine kama kupunguza vifo vya kina mama wakati wa kujifungua na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

Amesema wanawake wameathirika zaidi na mdororo wa uchumi huku milioni 18 miongoni mwao wakikosa ajira kwa mujibu wa shirika la kazi duniani ILO. Amesema lazima wanawake wapewe haki zinazostahili katika masuala yote na kitengo chake kitajitahidi kuhakikisha hilo na kuchagiza usawa katika ushiriki wa wanawake kwenye siasa.