Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ameteua tume kusimamia kura ya maoni Sudan na Abyei

Ban ameteua tume kusimamia kura ya maoni Sudan na Abyei

Kwa kujibu ombi la pande zinazounga mkono makubaliano ya amani ya Sudan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameteua tume ya kuangalia kura ya maoni ya Sudan Kusini na eneo la Abyei.

Ban Ki-moon amemteuwa Rais wa zamani wa Tanzania bwana Benjamini Mkapa kuongoza jopo hilo. Wajumbe wengine ni Bwana Antonio Monteiro waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ureno na bwana Bhojraj Pokharel mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi ya Nepal. Tume hiyo itazuru mara kadhaa Sudan hadi wakati wa kura hiyo iliyopangwa kufanyika Januari 2011, na itashirikiana na pande zote husika katika mkataba wa amani, tume ya kushughulikia kuara ya maoni, jumuiya za kiraia na makundi ya waangalizi wa kura hiyo.

Tume hiyo itafuatilia kwa karibu mchakato mzima wa kura ya maoni na pia masuala ya kisiasa na hali ya usalama. Mbali ya kuwasilisha taarifa kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa tume hiyo itafanya kazi kuhakikisha inaimarisha imani ya mchakato wa kura ya maoni kwa kuzichagiza pande husika na viongozi kuchukua hatua za pamoja kutatua matatizo yoyote au migogoro itakayojitokeza.

Kura ya maoni Sudan Kusini ni ya muhimu sana kwa ajili ya hatma ya nchi nzima ya Sudan. Katibu Mkuu amesema ana imani kwamba tume aliyoteua itasaidia katika kuchagiza kuwepo kwa kura ya maoni itakayozingatia matakwa ya watu wa Sudan Kusini na eneo la Abyei. Umoja wa Mataifa unatoa msaada muhimu kupitia mpango wake nchini Sudan UNMIS wa vifaa, kiufundi na usalama katika kura zote mbili za maoni.