Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani mauaji ya waandishi habari Pakistan

UNESCO yalaani mauaji ya waandishi habari Pakistan

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi, elimu na utamaduni UNESCO ambalo pia linaangalia uhuru wa habari leo amelaani mauaji ya waandishi wawili wa magazeti nchini Pakistan na kutoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kuwachukulia hatua waliotekeleza mauaji hayo.

Bi Irina Bokova amesema Mujeebur Rehman Saddigui mwenye miaka 39 ambaye ni mwandishi wa gazeti la Daily Pakistan alipigwa risasi na kuuawa na mtu asiyejulikana Septemba 16 alipokuwa akitoka msikitini kwenye jimbo la magharibi la KPK.

Naye Misri Khan Orakzai mwenye miaka 48 aliyekuwa mwandishi wa magazeti kadhaa ya nchi hiyo likiwemo la Islamabad Jinnaj na la Peshawar Mashriq aliuawa kwenye jimbo hilohilo September 14, na alipigwa risasi na watu watatu wasiojulikana.

Bi Bokova amesema serikali lazima iwakamate na kuwachukulia hatua zinazostahili waliofanya mauaji hayo, kwani ni kinyume cha sheria na wanakandamiza uhuru wa habari.