Skip to main content

Haki za binadamu ni muhimu kwa malengo ya milenia:UM

Haki za binadamu ni muhimu kwa malengo ya milenia:UM

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu awaambia viongozi wa dunia kuwa suala la haki za binadamu halikwepeki ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia

Wakati zaidi ya viongozi 100 duniani wanakutana Mjini New York Marekani kuudhuria mkutano wa malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa , Kamishna mkuu wa Umoja huo wa Mataifa juu ya haki za binadamu amewakumbusha viongozi hao namna wanavyoweza kufikia shabaya ya kuyafikia malengo hayo kwa kutoyapa kisogo masuala ya haki za binadamu.

Kamishna Mkuu wa Umoja huo wa Mataifa juu ya haki za binadamu Navi Pillay amesema kuwa nchi wanachama wa Umoja huo zinaweza kupiga hatua kubwa na kuyafikia malengo hayo ya mellenia iwapo kama zitachukua mkondo unaokubalika na kuzingatia masuala ya haki za binadamu.

Amesema kuwa kimsingi viongozi wengi wameendelea kuwa hodari wa kuweka ahadi lakini chakushangaza wengi wao wameshindwa kuzitekeleza ahadi hizo kwa vitendo jambo ambalo amesisitiza kuwa linavunja moyo hasa kipindi hiki ambacho viongozi hao wanakutana kwa ajili ya kufanya tathmini ya namna walivyopiga hatua kuyafikia malengo ya milenia.