Dola zaidi ya bilioni 2 zimeombwa leo kwa ajili ya Pakistan

Dola zaidi ya bilioni 2 zimeombwa leo kwa ajili ya Pakistan

Ikiwa ni chini ya miezi miwili tangu maruriko makubwa kuikumba Pakistan, Umoja wa Mataifa na washirika wale leo wamezindua ombi la zaidi ya dola bilioni mbili ili kutoa msaada kwa watu wapatao milioni 14 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Ombi hilo ni la kutekeleza miradi 483 itakayoongozwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa , shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali 156 ambayo ni ya kitaifa na kimataifa. Ombili hili linafuatia lile la awali la msaada wa dola milioni 459.7 lililotolewa Agosti 11.

 Mafuriko nchini Pakistan yameathiri watu zaidi ya milioni 20 ikiwa ni asilimia 10 ya watu wote. Mafuriko hayo yaliyoathiri eneo la kilometa 160,000 kubwa kuliko nchi ya England limekatili maisha ya watu zaidi ya 1700, kuharibu miundombinu na kubomoa nyumba karibu milioni 1.9.