Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waonya mauji na utekaji wakati Afghanistan ikijiandaa na uchaguzi

UM waonya mauji na utekaji wakati Afghanistan ikijiandaa na uchaguzi

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Staffan de Mistura amelaani vikali mauwaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya maafisa wawili wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo.

Maafisa hao waliuwawa katika jimbo la Charbolak lililopo Kaskazini mwa nchi hiyo, na tukio hilo limekuja wakati faifa hilo likijiandaa na uchaguzi wake mkuu Septemba 18 mwaka huu. Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kabul,mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa anaungana na Mwenyekiti wa tume ya taifa nchini humo kulaani mauwaji hayo ambayo ameyaita ya kinyama na yasiyokubalika.

Amesema vitendo vya kutishia uhuru na utendaji kazi wa watumishi wa tume ya uchaguzi, haviwezi kuvumiliwa na kutaka vikomeshwe mara moja. Hata hivyo afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Umoja wa Mataifa bado utaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi wa Afghanistan na ni matumaini ya Umoja wa Mataifa uchaguzi ujao utafanikiwa.