Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua:UNICEF

Vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua:UNICEF

Makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu vifo vya watoto inaonyesha mafanikio katika kupunguza idadi ya watoto wanaokufa kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa makadirio hayo yaliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF idadi ya watoto wa chini ya miaka mitano wanaokufa imepungua kutoka watoto milioni 12.4 hadi watoto milioni 8.1 kwa mwaka kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 2009. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Makadiriro hayo pia yanaonyesha kuwa vifo vya watoto vilipungua kwa thuluthi moja kwa kipindi hicho kutoka watoto 89 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa hadi watoto 60 ilipotimia mwaka 2009. Hata hivyo kuna changamoto kubwa za jinsi ya kuzuia vifo vya watoto hasa inapobainika kuwa kwa sasa watoto 22,000 walio chini ya miaka miatano hufa kila siku kote duniani wakati asilimia 70 kati yao wanapokufa mwaka wa kwanza baada ya kuzaliwa.

Kulingana na makadirio hayo eneo lililo kusini mwa jangwa la sahara linaandikisha asilimia kubwa ya watoto wanaokufa kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano ambapo mtoto mmoja hufa kwa kila watoto wanane wanaozaliwa ikiwa na mara ishirini zaidi na nchini ziliozostawi ambapo ni mtoto mmoja tu hufa kwa kila watoto 167 walio chini ya miaka miatano.