Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zimepigwa katika vita dhidi ya ukimwi Afrika

Hatua zimepigwa katika vita dhidi ya ukimwi Afrika

Takwimu mpya za shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS zimesema hatua zimepigwa katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara katika kupunguza maambukizi mapya ya HIV.

UNAIDS inasema nchi 22 ambazo zimeathirika zaidi Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara zimefanikiwa kupunguza maambuzi mapya kwa zaidi ya asilimia 25 na kutoa matumaini ya kutimiza lengo namba 6 la maendeleo ya milenia .

Takwimu hizo ambazo zimetolewa siku chache kabla ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuanza kikao chake kitakachojadili malengo ya maendeleo ya milenia wiki ijayo zinasema nchi zilizokuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi kama Ivory Coast, Ethiopia, Nigeria, Afrika ya Kusini, Zambia na Zimbabwe kwa sasa ndio zinazoongoza katika kupunguza maambukizi mapya.

(SAUTI YA DR UNAIDS )

Michele Sidibe mkurugenzi mkuu wa UNAIDS amesema hata hivyo bado kuna changamoto, kwani Ulaya mashariki na Asia ya kati wanaendelea kupata maambukizi na katika baadhi ya mataifa tajiri kumekuwa na maambukizi kwa wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja. Kwa sasa kuna watu milioni 5.2 wanaopata dawa za HIV ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 katika kipindi cha miaka sita.